
Kama chombo kinachosimamia uendeshaji wa
mpira wa miguu nchini, TFF imesikitishwa na habari hizo na inaiomba
klabu ya Yanga kufanya kila jitihada kuhakikisha kuwa
inawasilishataarifa zote muhimu na nyaraka zinazohusiana na stahiki za
kocha huyo ili kama ilishamalizana naye, sifa ya klabu ya Yanga
isafishwe. Tayari barua imeshaandikwa kwa klabu ya Yanga kuitaka
itekeleze utashi huo mapemz iwezekanavyo.
Tukio hilo, si tu linachafua sifa ya
klabu ya Yanga, bali soka ya Tanzania kwa ujumla kutokana na ukweli
kwamba ikishadhihirika kuwa kuna tatizo la malipo ya makocha nchini, ni
dhahiri kuwa itakuwa ni vigumu kwa klabu zetu na hata timu za taifa
kupata makocha wazuri kutoka nje kwa kuwa watakuwa wamejengeka hofu ya
kufanya kazi nchini.
Hili ni tukio la pili kwa Yanga baada ya
mchezaji wake mwingine, John Njoroge kuishtaki klabu hiyo FIFA na
kushinda kesi yake iliyoamuliwa mwezi Januari na Kitengo cha Usuluhishi
wa Migogoro cha FIFA (DRC). Ushindi wa Njoroge unamaanisha kuwa iwapo
Yanga itashindwa kutekeleza kumlipa mchezaji huyo kasi cha Sh milioni
17, inaweza kujikuta katika adhabu ambayo itatulazimisha tuishushe
daraja; kuinyang’anya pointi kwa kiwango kitakachotajwa na FIFA;
kuipiga faini au adhabu zote kwenda kwa pamoja. Tunaiomba Yanga
itekeleze hukumu hiyo kwa wakati uliotajwa kwenye barua ya FIFA ili
kuepuka hatua hizo.
Suala la Njoroge ni moja kati ya matukio
mengi yanayohusu ukiukwaji wa taratibu za kuvunja mikataba yanayofanywa
na klabu zetu. Kuna malalamiko ya wachezaji wengi dhidi ya klabu zao za
zamani kuhusu kutolipwa stahiki zao. Hivyo TFF inatoa wito kwa klabu
kujiepusha na vitendo hivyo kwa kuwa vinawanyima haki wachezaji, lakini
pia vinachafua sifa ya nchi iwapo wachezaji wanachukua hatua za kwenda
kwenye vyombo vya juu.
Tumekuwa tukisoma kwenye vyombo vya
habari kuhusu kutimuliwa kwa sekretarieti nzima ya Yanga kutokana na
kuonekana kuwa ina udhaifu. Taarifa hizo hazijaifikia rasmi TFF.
Kiutaratibu, Yanga inatakiwa iwsasilishe majina ya maofisa watakaofanya
kazi na TFF kwa sasa na itakapoajiri sekretarieti ya kudumu, basi itume
barua nyingine ya kuwatambulisha watendaji wake.
Kama itakuwa imeitimua sekretarieti
nzima, basi TFF inapokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa. Si nia ya
TFF kutetea watendaji wazembe, lakini klabu hazina budi kufuatilia kwa
karibu utendaji wa sekretarieti zao ili isije ikafikia wakati
sekretarieti nzima inaondolewa kwa makosa ambayo yangeweza kusahihishwa
kama kungekuwa na ufuatiliaji wa karibu. TFF imekuwa ikitoa mafunzo kwa
watendaji wa klabu ili waweze kufanya kazi zao vizuri na kwa mintaarafu
ya mpira wa miguu na hivyo kuondolewa kwa timu nzima kama hiyo
kunamaanisha kuwa ni upotevu wa rasilimali ambayo imetumika kuwapa elimu
ya kutenda kazi zao vizuri. TFF ilishafanya kozi ya Event Management
kwa ajili ya watendaji wa klabu; semina ya kuangalia upya maazimio ya
Bagamoyo kwa watendaji na viongozi na pia kozi ya utawala hivyo haipendi
juhudi hizi zipotee kirahisi.
Angetile Osiah
KATIBU MKUU
++++++++++
Release No. 154
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Septemba 25, 2012
LIGI KUU VODACOM KUENDELEA KESHO
Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom kuwania
ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho (Septemba 26 mwaka huu) kwa
mechi mbili zitakazochezwa katika miji ya Tanga na Morogoro.
Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro utakuwa
mwenyeji wa mechi kati ya Polisi Morogoro na Toto Africans ya Mwanza.
Polisi Morogoro ambayo imepanda daraja msimu huu imeshacheza mechi tatu
na kufanikiwa kupata pointi moja tu baada ya kutoka suluhu na Mtibwa
Sugar katika mechi ya kwanza.
Nayo Toto Africans ambayo katika mechi
iliyopita ugenini ililazimisha suluhu dhidi ya Coastal Union, yenyewe
ina pointi tatu baada ya kutoka sare katika mechi zote tatu ilizocheza
chini ya kocha John Tegete.
Mechi nyingine ya ligi hiyo itakuwa kati
ya Coastal Union ambayo itaikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa
Mkwakwani jijini Tanga. Kagera Sugar inayofundishwa na Abdallah Kibaden,
wikiendi iliyopita iliondoka na pointi zote tatu kwenye uwanja huo
baada ya kuifunga Mgambo Shooting bao 1-0.
Ligi hiyo itaingia kwenye Super Weekend
kuanzia Ijumaa (Septemba 28 mwaka huu) kwa mechi kati ya Azam na JKT
Ruvu itakayochezwa Uwanja wa Taifa itaoneshwa moja kwa moja (live) na
kituo cha SuperSport kuanzia saa 1 kamili usiku.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 comments: