TIMU ya
taifa, Taifa Stars itaanza kampeni ya kuwania kufuzu kucheza fainali za
Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan) dhidi ya timu
ya Taifa ya Uganda (The Cranes). Fainali hizo zimepangwa kuchezwa nchini Afrika Kusini mwaka 2014. Taifa Stars itaanza mchakamchaka huo kwa mechi ya kwanza kuchezwa nyumbani, kabla ya kusafiri kwenda Uganda kwa ajili ya mechi ya marudiano Juni 23, mwakani. Tanzania ilishindwa kufuzu kwenye fainali zilizopita, baada ya kufungwa na Rwanda katika hatua za awali za mashindano hayo. Kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) mjini Cairo, Misri katikati ya wiki hii, inaonyesha kuwa Rwanda itacheza na mshindi kati ya Eritrea na Ethiopia zitakazoanzia hatua ya mtoano. Burundi na Kenya zitacheza hatua ya mtoano Novemba 30, huku Sudan ikisubiri kupambana na mshindi wa mechi hiyo. Michuano hiyo itashirikisha nchi 38. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ilitwaa taji la kwanza mwaka 2009, na 2011 taji hilo lilikwenda Tunisia. Wakati huohuo, wachezaji Abuu Zuberi Ubwa na Hamisi Thabit Mohamed wameombewa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) na Shirikisho la Soka Ureno (FPF) kwa ajili ya kucheza soka la kulipwa. Wachezaji hao ambao kwa nyakati tofauti waliwahi kucheza Yanga ya Dar es Salaam na kushindwa kung'ara wameombewa ITC kama wachezaji wa ridhaa. Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema jana kuwa wanasoka hao watajiunga na klabu ya Atletico Sport Clube ya Ureno, ambayo hata hivyo haikuelezwa iko daraja gani nchini humo. "FPF imeombwa kupatiwa hati ya maelezo ya kila mchezaji zikiwamo taarifa za ushiriki wao katika mechi rasmi zinazotambuliwa na TFF wakiwa katika klabu zao hizo za zamani," alisema Wambura |
0 comments: